Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho anatarajiwa kuongoza mrengo wa upinzani wa Cord katika maandamano ya amani dhidi ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC siku ya Jumatatu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo la Mtopanga, Gavana Joho aliwataka wafuasi wa Cord kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maandamano hayo.

“Tunataka kuandaa maandamano ya amani na tunatarajia kuwa maafisa wa polisi watatupa usalama wa kutosha tutakapoenda kuwasilisha malalamishi yetu katika afisi za IEBC,” alisema Joho.

Akiwahutubia wanahabari afisini mwake, mwenyekiti wa chama cha ODM Mohammed Khatmy, alisema kuwa viongozi wote wa Cord wakiwemo Gavana Joho na Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar wanatarajiwa kushiriki maandamano hayo yatakayoanza saa nne asubuhi katika bustani la Uhuru.

Khatmy alitoa onyo kwa wafuasi wa mrengo huo kwa kusema kuwa hali yoyote ya vurugu haitakubaliwa katika maandamano hayo.

Mwenyekiti huyo aliema kuwa maafisa wa polisi watakuwa macho ili kuzuia wahuni ambao watatumia fursa hiyo katika kutekeleza matendo yasiyohalali.

Siku ya Jumamosi, kiongozi wa chama cha Wiper ambaye pia ni mmoja wa viongozi katika mrengo wa Cord Kalonzo Musyoka, aliwaagiza waandamanaji wote kufika katika maandambano hayo siku ya Jumatatu na vitambaa vyeupe ili kuashiria maandamano ya amani.