Seneta mteule wa Kaunti ya Mombasa Emma Mbura amewashinikiza Kamishna wa kaunti ya Mombana Nelson Marwa na Gavana Hassan Joho kujitokeza na kuwatia nguvuni walanguzi wakuu wa dawa za kelevya.
Kulingana na Mbura, tangu oparesheni ya kuwasaka walanguzi wa dawa za kulevya katika kaunti hiyo na eneo zima la pwani kuanzisha rasmi na Rais Uhuru Kenyatta, hakujawahi kamatwa mlanguzi mkuu hata mmoja wa dawa za kulevya ili kuonesha kwamba juhudi hizo zinafaulu.
Akiwahutubia wakazi wa mjini Mombasa siku ya Jumanne katika sherehe za siku ya mashujaa, Mbura alisema kwamba lazima walanguzi hao watiwe nguvuni ili kusitisha kuena kwa biashara hiyo haramu.
Alisema kuwa wanaoathirika zaidi ni vijana wadogo huku akiwakosa viongozi hao kwa kuwatia nguvuni waathiriwa wa mihadarati ambao wanahitaji matibabu ili kujinasua.
“Ni lazima viongozi wetu kujitokeza kikamilifu na kuwatia nguvuni walanguzi wakuu wa mihadrati ili kuwanasua vijana wetu kutoka janga hilo. Tabia ya maafisa wa polisi kuwakamata waathiri yapaswa kukomeshwa kwasababu hawa vijana wanahitaji matibabu sio kuweka kizuizini,” alisema Mbura.
Wakati uo huo alimtaka Gavana Joho kutenga sehemu maalum ya kuwasaidia vijana kufanya shughuli zao za kimaendeleo, na kupendekeza jumba la kuhifadhi bidhaa za kaunti hiyo katika eneo la Buxtan mjini Mombasa.
Kauli ya Seneta huyo ilijiri baada ya wakazi kulalama kuwa idadi kubwa ya vijana wanaotiwa nguvuni na maafisa wa polisi hawahusiki na biashara hiyo haramu katika kaunti hiyo ya Mombasa.