Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amemtaka Gavana Hassan Joho kuasi siasa za vitimbi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Omar amesema kuwa sharti Gavana Joho aangazie masaibu yanayowakabili wakaazi wa Mombasa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena mjini Mombasa, Omar alisema imekuwa kama desturi kwa Joho kutumia wadhifa wa naibu kiongozi wa chama cha ODM kuwaalika wasanii mashuhuri kwenye mikutano ya kisiasa.

Omar aliikosoa hatua hiyo kwa kusema kuwa Joho anawakandamiza wakaazi wa Mombasa kwa kuwaburudisha kwa muda mfupi kisha baadaye wanarejea kuishi kwenye lindi la umaskini, ambalo alilitaja kama janga kubwa linalokumba Mombasa.

Omar alidai kuwa Joho hana lolote la kujivunia kwa wakaazi tangu kuingia mamlakani, huku akisema kuwa miradi mingine imesalia kuwa matamshi vinywani mwa wakaazi.

Alisema kuwa kinachoonekana kwa sasa ni burudani na vitimbi vya kila aina vya kutaka kuwaziba macho wananchi.

Omar ni baadhi ya viongozi kutoka Mombasa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuukosoa utendakazi na uongozi wa Joho, haswa miradi iliyoanzishwa na serikali ya kaunti.