Seneta wa Mombasa Hassan Omar amemkashifu Gavana Hassan Joho kwa kumpigia upato Raila Odinga bila kuzingatia vinara wengine katika muungano wa Cord.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Omar amesema kuwa swala la Joho kuwania urais mwaka wa 2022 utaathiri uhusiano katika muungano huo.

katika kikao na waandishi wa habari jijini Mombasa siku ya Jumatatu, Omar ambaye ni kinara wa chama cha Wiper alisema kuwa chama hicho kiko tayari kumuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga, ikiwa watakubaliana na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na kinara wa Ford Kenya Moses Wetangula.

"Wakati sisi tunatafuta mbinu za kung'oa Jubilee mamlakani, yeye (Joho) tayari ashaanza kampeni zake za 2022. Kama huo si ubinafsi basi ni nini?" aliuliza Omar.

Hata hivyo, seneta huyo alisema kuwa iwapo watakubaliana kumuunga mkono Raila, basi ni lazima mkataba uafikiwe ili Raila amuunge mkono Kalonzo ama Wetangula katika uchaguzi wa 2022, na wala sio kumuunga mkono Joho.

Haya yanajiri huku chama cha Wiper kikijitayarisha kuandaa mkutano wa washikadau jijini Nairobi ili kujadili hatma ya chama hicho katika mrengo wa Cord.