Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema hawezi kuomba msamaha Rais Uhuru Kenyatta baada ya kudaiwa kumshutumu hadharani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizumgumza siku ya Jumatano katika ukumbi wa Bomas wakati wa mkutano wa vyama vya upinzani, Joho alisema kuwa alimwambia Rais Kenyatta ukweli kuhusu miradi ya Jubilee Kaunti ya Mombasa, na kuongeza kuwa atazidi kuweka wazi hadharani kuwa Jubilee haijafanya miradi yoyote Mombasa.

Wakati huo huo, Joho alisema hana haja ya ulinzi na kuitaka serikali ya Jubilee kutwaa walinzi wake.

Aliongeza kuwa yuko huru na hatishiki kutembea bila ya walinzi wa serikali ya Jubilee.

“Nimetembea mwenyewe leo bila walinzi wowote. Sihitaji walinzi kwa kuwa nina amini Mungu atanilinda,” alisema Joho.

Aidha, gavana huyo amesemakuwa raia wake watamlinda na usalama wake uko shwari.

Haya yanajiri baada ya idara ya usalama siku ya Jumanne kutangaza kuwaregeshea Gavana Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi walinzi wao.