Gavana wa Mombasa Hassan Joho ameikashifu serikali ya Jubilee kwa madai ya kuhusika katika wizi wa mali ya umma.
Akihutubia wakaazi wa Kaunti ya Bomet siku ya Jumamosi, Gavana Joho aliikosoa serikali kuu kwa madai ya kutumia kiwango kikubwa cha fedha katika ujenzi wa barabara maeneo mbalimbali nchini.
Joho alidai kuwa serikali ya Jubilee imeongeza gharama ya miradi hiyo ya barabara mara dufu.
“Ndungu zangu (Jubilee) wanatembea wakisema wanaleta miradi. Tumefanya utafiti na kugundua kwamba miaka mitatu iliyopita, ujenzi wa barabara ulikua unagharimu bei nusu ya mwaka huu,” alisema Joho.
Joho, ambaye ni kiongozi naibu wa chama cha ODM, alidai kuwa Naibu Rais William Ruto anatumia fedha za umma kujenga nyumba yake.
“Nawauliza watu wa Bomet, ile pesa Ruto amechukua kujenga nyumba ya shilingi billioni moja, munalala naye katika nyumba hiyo?” aliuliza Joho.
Aidha, alisema kuwa hatachoka kuwakashifu na kuwakosoa viongozi wanaoiba mali ya umma.
“Kule mimi natoka, mtu mwizi tunamuita mwizi. Mimi Hassan Joho siwezi kutishwa na mtu mwizi. Mimi ndiye nitatisha mwizi,” alisema Joho.