Aliyekuwa mshukiwa katika kesi ya uchochezi wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 Joshua Arap Sang ametangaza nia yake ya kurejelea uanahabari baada ya miaka minane sasa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hii ni baada ya kesi dhidi yake kutupiliwa mbali juma liliopita kufuatia ukosefu wa ushahidi kwa upande wa mashtaka.

Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye mahojiano na Radio Taifa, Bwana Sang alidokeza kuwa ataanzisha stesheni ya runinga na redio itakayopeperusha matangazo ya injili ya kikristu kwa lugha ya Kiswahili ni Kiingereza.

"Nitarejea kwenye uanahabari kwa kuanzisha stesheni ya redio na runinga itakayoangazia injili ya kikristu hivi karibuni kwa ushirikiano na marafiki wangu, ili kueneza injili ya mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kuwa huru baada ya miaka minane," alisema Sang.

Bwana Sang aliilezea kupoteza imani yake kwa Mahakama ya ICC baada ya upande wa mashtaka kufanya uchunguzi hafifu uliochangia kutupiliwa mbali kwa kesi dhidi ya washukiwa wote sita, na kuchangia pakubwa kufifia kwa matumaini ya haki kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Aidha, Sang alidokeza kuwa ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali ya sasa katika kushughulikia waathiriwa hao licha ya kuwa mathara ya ghasia hizo kukosa kusahaulika.

Akiangazia azimio lake la kisiasa, Bwana Sang alisema kuwa anajadiliana na viongozi na wendani wa karibu ili kufanya uamuzi dhabiti kwa nia yake ya kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Sang amewataka viongozi nchini kujiandaa kukubali hatma yoyote ile katika uchaguzi mkuu ujao na kuwaomba vijana kujiepusha na yeyote anayechochea chuki na kuvuruga amani nchini Kenya.