Wajumbe wa amani kwenye mkutano wao siku ya Jumanne mjini Mombasa. Picha: Otieno O/ hivisasa.com
Joto la kisiasa linalozidi kupanda hasa katika Kaunti ya Mombasa sasa limeanza kuwatia hofu makundi mbalimbali ya kutetea amani na haki za kibinadamu.Siki ya Jumanne, kamati ya amani na uwiano Kaunti ya Mombasa ilijitokeza na kuwataka viongozi wa kisiasa kuwa makini na matamshi wanayotoa wakati wa kampeni hasa wakati huu ambapo siasa zinazidi kuchacha.Kamati hiyo imesema mizozo na misururu ya mikutano ya kisiasa inayofanywa Mombasa na mirengo mbalimbali ya kisiasa inaweza kuwa hatari kwa usalama wa wakaazi na hata kwa sekta ya utalii.Shamsa Abubakar, mmoja wa wanakamati hao, amewataka wakaazi kudumisha umoja na kutokubali kugawanywa na wanasiasa ambao wanapigania maslahi yao ya kibinafsi.“Wakaazi wa Mombasa tuwe na subira sana, tuwe makini sana msimu huu wa mawimbi ya siasa. Mambo ya siasa yatakuja na kwenda lakini Kenya itasalia kuwa yetu hivyo tusikubali kugawanywa,’’ alisema Bi Shamsa.Kwa upande wake, mkurugenzi wa shirika la kijamii la KECOSCE Phyllis Muema amewataka viongozi wa kisiasa Mombasa kuhubiri amani katika mikutano yao badala ya kutoa matamshi yanayoweza kugawanya wakaazi.“Nawahimiza viongozi wetu wa kisiasa kuzingatia ubusara katika semi zao, muda huu si wa kufanya mzaha kwani taifa linahitaji umoja wala sio mgawanyiko,” alisema Bi Muema.Kaunti ya Mombasa imeshuhudia mikutano miwili mikubwa katika mwezi Machi, vyama vya Jubilee na ODM vyote vikiandaa mikutano yake katika uwanja wa Tononoka kujipigia debe.Aidha, malumbano ya mara kwa mara baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Gavana Joho pia yanatajwa kuwakera wakaazi.