Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Joto la kisiasa tayari limeanza kutanda kwenye kaunti ya Nakuru huku viongozi mbalimbali wakijitokeza kuweka wazi kwamba watawania viti mbalimbali vya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya wale ambao wamejitokeza wazi wameelezea azma yao ya kuwania kiti cha ugavana kwenye kaunti ya Nakuru na kile cha mwakilishi wa akina mama kwenye kaunti hii.

Miongoni mwa wale ambao wamejitokeza hadharani ni waziri wa kilimo kwenye kaunti ya Nakuru ni Purity Muritu aliyeweka wazi azma hiyo kwenye mkutano wa maombi wa kutakasa soko la Wakulima lililo mjini Nakuru uliofanyika Ijumaa hii ya tarehe 22 Januari.

Kwa upande mwingine, kiongozi mwingine kwa jina la Zipporah Kimani aliyewania kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013 na kushindwa pia amesema kuwa atawania kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.

Wakati uo huo, Muritu aliwasihi wananchi kuchagua viongozi walio na rekodi ya utendakazi na wala sio wale wanotoa tu hadai na kukosa kuzitimiza.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nakuru pia ameweka bayana kuwa atawania tena kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Aidha, wale ambao wamejitokeza kutangaza kuwa watawania kiti cha ugavana kwenye kaunti ya Nakuru katika uchaguzi mkuu ujao ni pamoja na mwenyekiti wa halmashauri ya usafiri na usalama wa barabarani NTSA Lee Kinyanjui, mwenyekiti wa shirika la kukabiliana na utumizi wa dawa haramu na pombe Nacada John Mututho na gavana wa sasa wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua.