Hatua ya muungano wa Jubilee kuunganisha vyama tanzu vinavyounda muungano huo na kuwa chama kimoja kipya cha Jubilee, inazidi kuzua hisia mseto miongoni mwa wanasiasa nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa chama cha ODM Kaunti ya Mombasa Mohammed Hatimy amesema hatua hiyo inarejesha taifa katika enzi za ukoloni, kwa kuwa inakiuka uhuru wa kuwa na vyama vingi.

“Jubilee itaturejesha katika enzi za ukoloni. Hapa kuna karata inachezwa na lazima watu wawe makini. Tunarudi katika siku zile chama cha KANU - chama cha mama na baba ambapo mtu hangeruhusiwa kutoa maoni yake au msimamo wake hasa unaopinga uongozi uliopo madarakani,” alisema Hatimy.

“Hii ni kama kuua uhuru wa watu kutaka kujisimamia kisiasa kulingana na maoni na mawazo yao na badala yake kuwanufaisha watu wachache wenye nia ya kujifaidi kwa kuwatumia wengine,” aliongeza.

Hatimy vilevile ametofautiana na kauli ya Jubilee kuwa chama kimoja kitaleta umoja nchini akisisitiza kuwa hatua hiyo itazua mvurugano baina ya viongozi wa kisiasa hasa wakati wa uteuzi wa wawaniaji viti mbalimbali vya kisiasa.

“Hii mambo ya chama kimoja kitaleta mgawanyiko mkubwa nchini hasa miongoni mwa viongozi wa kisiasa. Kila mtu atataka kugombea nyadhifa ya kisiasa na ikiwa atafungiwa kwa kuwa chama ni kimoja huenda kukatokea malumbano kwani watataka kuhamia vyama vingine kutimiza ndoto zao,” aliongeza Hatimy.

Muungano wa Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto siku ya Jumanne ulizindua mpango wa kuvunjilia mbali vyama tanzu vyake na kuunda chama kimoja cha Jubilee utakaotumia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Vyama hivyo tanzu takribani 12 vitavunjwa kuunda chama cha Jubilee rasmi tarehe nane mwezi Septemba.