Waziri wa Utalii nchini Najib Balala amesema kuwa serikali ya Jubilee itasalia madarakani hadi mwaka wa 2032.
Balala ambaye alikuwa akizungumza katika kongamano la wadau katika sekta ya utalii iliyofanyika jijini Mombasa siku ya Alhamisi, alisema kuwa tayari wizara hiyo ilikuwa imeweka mikakati ya kuinua sekta hiyo kwa miaka kumi ijayo, kwa matumaini kuwa serikali ya Jubilee itaongoza nchi kwa muda huo wote.
“Tuna matumaini kuwa tutachaguliwa kama serikali ya Jubilee katika uchaguzi mkuu ujao na baada ya hapo Naibu wa Rais William Ruto atachukua usukani,” alisema Balala.
Aidha, Balala alitoa changamoto kwa serikali ya Kaunti ya Mombasa kusafisha mji huo, akisema kuwa taka ambazo zimetapakaa kila mahali zitaletea jiji hilo sifa mbaya.