Viongozi wa Jubilee wamekanusha madai kuwa chama hicho kinapanga kuiba kura, kufuatia hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuwapa wanachama cha jamii ya Makonde vitambulisho.
Wakiongozwa na mwanasiasa Ibrahim Babangida, viongozi hao walisema kuwa Rais Kenyatta alichukua hatua hiyo ili kusaidia jamii hiyo, kwani ilikuwa imeteseka kwa muda mrefu bila kutambulika kama Wakenya.Babangida alisema kuwa chama hicho hakina njama yoyote ya kuiba kura katika uchaguzi wa Agosti, kwani lengo lao kuu ni kuwa na uchaguzi wa huru na haki.Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Babangida aliwataka viongozi wa kisiasa humu nchini kukoma kuingiza siasa katika swala hilo, kwani huenda likazua hofu miongoni mwa wananchi.Aidha, amewahimiza viongozi kuendeleza kampeni zao katika njia itakayoleta Wakenya pamoja wala sio kuleta mgawanyiko.Wakati huo huo, amewataka wakaazi wa Mombasa na ukanda wa Pwani kwa jumla kujitokeza kwenye zoezi la kusajili wapiga kura linalotarajiwa kutamatika hivi karibuni.
Maelezo ya picha: Rais Uhuru Kenyatta akiwapa wanachama wa jamii ya Mokonde vitambulisho hapo awali.
Picha/PSCU.