Viongozi wa Jubilee Kaunti ya Mombasa wamekanusha madai kuwa chama hicho kinanunua na kuwahamisha wakaazi wa maeneo mengine na kuwapeleka kujiandikisha kama wapiga kura katika ngome za Cord eneo la Pwani.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Suleiman Shahbal, ambaye ni mgombea wa kiti cha ugavana Kaunti ya Mombasa, amepuzilia mbali madai hayo kwa kusema kuwa ni uvumi usiokuwa na msingi.

Akizungumza siku ya Jumapili katika uwanja wa Tononoka, Shahbal ameutaja uvumi huo kama ishara ya kushindwa kwa mrengo wa upinzani katika uchaguzi ujao.

“Viongozi wa upinzani wameanza kutetemeka na kuanza kuzua madai yasiyokuwa na msingi wowote,” alisema Shahbal.

Aidha, Shahbal alisema kuwa Jubilee itazoa kura nyingi eneo la Mombasa katika uchaguzi wa Agosti.

“Nina uhakika kuwa Jubilee itazoa kura nyingi mwezi Agosti, kinyume na matarajio ya Cord,” alisema Shahbal.

Wakati huo huo, Shahbal alipinga madai kuwa Mombasa ni ngome ya Cord, na kusema kuwa wananchi wanahaki ya kupigia kura mrengo wowote, na kuitaka Cord kuacha kulalamika kabla ya uchaguzi.