Mfanyibiashara Josephine Kabura hii leo amefika mbele ya tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC ambapo anatazamiwa kutoa mwanga zaidi kuhusiana na hati kiapo inayomtaja waziri wa zamani wa ugatuzi Ann Waiguru kama mshukiwa mkuu kwenye sakata ya NYS.
Kabura alikosa kufika mbele ya tume hiyo juma lililopita kutokana na kile wakili wake aliifahamisha tume hiyo kuwa mteja wake alikuwa mgonjwa.
Mfanyibiashara huyo amefika mbele ya EACC kuhojiwa siku moja baada ya Waiguru kuhojiwa kwa muda wa saa kadhaa kuhusiana na tuhuma dhidi yake zilizoibuliwa kwenye hati kiapo hicho.
Hata hivyo waziri huyo wa zamani amekanusha kuwa hana uhusiano wowote na Kabura licha yake kudai kuwa Waiguru alifahamu vyema jinsi milioni 791 zilivyoptea kwenye shirika la vijana la NYS.
Hapo jana tume ya maadili na kupamabana na ufisadi EACC ilimhoji aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru kwa takribani saa tisa kuhusiana na sakata ya shilingi milioni mia saba tisini na moja ya shirika la kitaifa la vijana NYS.
Waiguru alifika mbele ya tume hiyo mwendo wa saa tano asubuhi na kuondoka muda mfupi baada ya saa mbili usiku, kutoa mwanga zaidi kuhusiana na anachokifahamau katika sakata ya kufujwa kwa fedha hizo za NYS.
Waiguru aliandamana na wafuasi wake hapo jana katika afisi za EACC ambapo alihojiwa na alibaki na msimamo kuwa hakuhusika na wizi wa fedha hizo za NYS.