Kadhi wa Kisumu Mursal Muhammed, amewashtumu wote wanaotekeleza ugaidi kwa jina la dini ya Kiislamu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muhammed alisema kuwa dini ya kiislamu, hairuhusu wala haifunzi kuua ama kutekeleza ugaidi.

Akizungumza na mwandsihi huyu afisni mwake jijini Kisumu siku ya Ijumma, Kadhi huyo alisema kuwa dini ya kiislamu ni ya amani, na inachukia ugaidi.

“Wale wote ambao wanatekeleza ugaidi kwa jina la dini ya ki-islamu, hawaelewi kamili mafunzo ya Kurani takatifu na pia wanafanya hivyo kwa manufaa yao wenyewe, bali sio kutimiza mafunzo ya kidini,” akakemea kadhi huyo.

Kadhi Muhammed, vile vile ameitaka serikali kuwakabili vikali wote wanaoshukiwa kufadhili ugaidi, au kushirikiana na magaidi.

Alisema kuwa hali ya kuwahusisha waislamu na ugaidi, inawadhalilisha waislamu na kuwafanya kutengwa katika jamii.

Matamshi ya kadhi huyo, yamejiri takribani majuma matatu baada ya wanamgambo wa Al Shabaab, kuvamia chuo kikuu cha Moi tawi la Garissa, na kusababisha mauaji ya watu 148, wengi wao wanafunzi; huku wengine wapatao 100 wakijeruhiwa.

Shambulizi hilo la tarehe mbili mwezi huu, ndio baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika ardhi ya Kenya, tangu kutokea kwa mlipuko wa bomu kwenye ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, mnamo mwaka 1998.

Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 211, huku wengine wapatao alfu nne wakipata majeraha mbali mbali.