Kadhi mkuu nchini Sheikh Ahmed Sharrif Muhdhar amewaomba waumini wa dini ya Kiislamu kote nchini kutowahanganisha wenzao kuhusu kuonekana kwa mwezi wa Ramadhan na badala yake kufuata maagizo kutoka kwa viongozi wa dini.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Sheikh Muhdhar, alisema kuwa waumini wa dini ya Kiislamu wanatarajiwa kuanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan siku ya Jumanne kutokana na kuwa mwezi bado haujaonekana.
Alisema kuwa mwezi unatarajiwa kuonekana masaa ya magharibi kufuatia kukamilika kwa siku ya 30 ya Shahbal mwaka wa 1437 mashariki ya kati kwa mujibu wa kalenda ya dini hiyo.
"Tunawaomba Waislamu wasilumbane kuhusu kuonekana kwa mwezi. Kama kawaida Ramadhan itaanza rasmi siku ya Jumanne baada ya kukamilika kwa siku 30 za Shahbal,” alisema Sheikh Muhdhar.
Aidha, amepinga madai ya kuonekana kwa mwezi katika maeneo ya Afrika Mashariki huku akiwaomba waumini wa dini ya Kiislam kuliombea taifa hilo wakati wa mwezi wa Ramadhan.