Idara za kupambana na ufisadi sawia na mashirika yaliyotwikwa majukumu ya kuchunguza kesi za ufisadi yametiwa dosari kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Haya ni kulingana na mwenyekiti wa mpango wa Nyumba Kumi nchini Joseph Kaguthi, aliyedokeza kwamba visa hivyo vya ufisadi vimeripotiwa kuongezeka maradufu katika nyanja mbali mbali katika serikali ya kitaifa na hata zile za kaunti.
Akionesha kutamaushwa kwake na mashirika hayo, Bw Kaguthi ameeleza kuwa visa vingi vya ufisadi vinaripotiwa na hata wanaotuhumiwa kushtakiwa katika mahakama mbali mbali nchini, ila huishia kuachiliwa huru muda mchache baadaye.
Alisema kuwa hali hiyo inashusha imani ya wananchi kwa idara hizo.
“Ni wazi mashirika haya yameshindwa kukabiliana na ufisadi nchini maana kila uchao visa vyaongezeka na hamna la maana linalotekelezwa,” alisema Kaguthi.
Akizungumza katika kongamano lililowaleta pamoja machifu jijini Mombasa, Kaguthi aliishinikiza serikali kutafuta mbinu mbadala ya kutatua tatizo la ufisadi nchini.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa iwapo visa vya ufisadi nchini vitakosa kuthibitiwa, wananchi wataendelea kukandamizwa kwa kukosa kupata maendeleo wanayostahili.
Itakumbukwa kuwa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa imeteuwa kila siku ya Alhamisi kama siku ya kufanya maadamano kama njia moja ya kuonesha kukereketwa kwao na maswala ya ufisadi nchini, huku wakiitaka serikali kuwajibika vilivyo katika vita hivyo.