Waziri wa Ardhi Jacob Kaimenyi amesema kuwa wizara yake inajitahidi kuangamiza na kuwakabili mabwanyenye wanaoendeleza unyakuzi wa ardhi za umma na kibinafsi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kaimenyi amesema kuwa wizara hiyo haitalegeza kamba kamwe katika kuzuia wananchi dhidi ya kunyanyaswa katika maswala ya ardhi.

Akizungumza kwenye kikao na wafanyakazi wa afisi za ardhi jijini Mombasa siku ya Jumatatu, Waziri huyo alisema kuwa atashirikiana na idara ya usalama katika kuwakamata mabwanyenye hao na kuwafikisha mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Tutawakamata hawa mabwanyenye wanaowahangaisha wananchi kwa kunyakua ardhi zao na kuwafikisha mahakamani ili wafungwe,” alisema Kaimenyi.

Aidha, amewaonya maafisa kutoka Wizara ya Ardhi dhidi ya kushirikiana na mabwanyenye katika kugushi vyeti na kuwanyanyasa Wakenya katika masuala ya ardhi.

“Tafadhali musishirikiane na hawa mabwanyenye katika kunyakuwa ardhi za Wakenya walala hoi,” alisema Kaimenyi.