Mwenyekiti mpya wa Shirika la huduma za feri KFS Ramadhan Kajembe ameelezea nia yake ya kuleta mabadiliko makubwa katika shirika hilo.
Kajembe, ambaye amewahi hudumu kama mbunge wa Changamwe alisema atahakikisha huduma bora zinatolewa ili kuridhisha kila Mkenya katika kivuko cha LIkoni.
Akizungumza na mwanahabari huyu muda mchache to baada ya tangazo la uteuzi wake siku ya Ijumaa, Kajembe aliahidi kufufua huduma za kivuko cha Mtongwe, ambazo kwa muda sasa zimekosekana.
Hali hiyo imetajwa kama sababu moja inayochangia msongamano mkubwa wa watu katika kivuko cha Likoni.
“Nitahakikisha kuwa ninaboresha huduma zote ili kuwafaidi raia katika kivuko hicho, kama njia moja ya kupunguza msongamano,” alisema Kajembe.
Kajembe pia alisema yuko imara kutatua changamoto zote zinazowakumba wafanyikazi wa shirika hilo ili kuwawezesha kujitahidi katika utoaji wa huduma bora kwa wasafiri.