Mbunge wa zamani wa Changamwe Ramadhan Kajembe ametangaza rasmi kustaafu siasa.
Kajembe amekuwa katika siasa kwa kipindi cha miaka 30, baada ya kuhudumu kama diwani kwa miaka 15 na kama mbunge kwa miaka 15.
Hata hivyo, Kajembe, ambaye ni mwenyekiti wa Shirika la Huduma za Feri (KFS) ameahidi kuunga mkono chama cha Jubilee kuhakikisha serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inateuliwa kwa mara ya pili katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nimestaafu siasa rasmi lakini bado ninaunga mkono Jubilee na nitazidi kupigia chama hicho debe,” alisema Kajembe.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa Jubilee uliofanyika katika uwanja wa Changamwe, Kajembe aliwataka Wakenya kupigia kura Jubilee kwenye uchaguzi ujao ili waweze kunufaika na miradi ya maendeleo.
“Pitisheni Jubilee na mutafaidika kimaendeleo. Wachana na muungano wa Cord kwani zao ni porojo na kelele,” alisema Kajembe.
Aidha, Kajemba amewataka Wakenya kujisajili kwa wingi kama wapiga kura ili kupata fursa ya kuchagua viongozi bora watakao tetea haki zao.