Aliyekuwa Mbunge wa Changamwe Ramadhan Kajembe ameteuliwa kama mwenyekiti wa Shirika la huduma za feri nchini KFS.
Kajembe ambaye alihudumu kama naibu waziri wa mazingira ni mmoja wa wanasiasa wakongwe katika eneo la Pwani, na aliwahi kuwania kiti cha useneta Kaunti ya Mombasa kupitia chama cha ODM na kushindwa na Seneta Hassan Omar wa Wiper.
Kiongozi huyo aliwahi kuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa chama cha ODM haswa katika kuendeleza sera za chama hicho eneo la Pwani kabla ya kukihama mapema mwaka jana na kujiunga na mrengo wa Jubilee.
Uteuzi wake unajiri baada ya shirika hilo kukumbwa na lalama tele kutoka kwa wananchi na wadau mbali mbali, kutokana na kudorora kwa huduma katika kivuko cha Likoni, hali iliyosababisha kusimamishwa kazi kwa meneja mkurugenzi Musa Hassan miongoni mwa mameneja wengine wawili.
Kajembe amechukua nafasi ya Mshenga Ruga.