Aliyekuwa mbunge wa Changamwe Ramadhan Kajembe ametoa wito kwa wakaazi wa eneo bunge hilo kuunga mkono serikali ya Jubilee ili irudi mamlakani mwaka ujao.
Kajembe alidai kuwa chama cha ODM kwa sasa hakina ajenda za maendeleo kwa wakaazi wa Pwani.
Akihutubia waumini katika kanisa la Jesus Church Ministry huko Changamwe, Kajembe alisem kuwa chama hicho cha upinzani hakina lolote la kuwapa Wakenya.
“Mimi sio mwanachama wa ODM tena. Nawaomba ndugu na kinadada muunge mkono chama cha Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta,” alisema Kajembe.
Kajembe aliwania kiti cha useneta Kaunti ya Mombasa kupitia tiketi ya chama cha ODM na kupoteza kwa Hassan Omar wa chama cha Wiper katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mapema mwaka jana, mwanasiasa huyo mkongwe alikihama chama cha ODM na kujiunga na Jubilee.
Kajembe aliteuliwa mwenyekiti wa Shirika la huduma za feri nchini KFS mwezi Juni.
Mgombea wa kiti cha ugavana kwa tiketi ya Jubilee Suleiman Shahbal aliunga mkono usemi wa Kajembe na kuahidi kuongoza kampeni za chama hicho katika eneo la Pwani, ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya chama cha upinzani cha ODM.