Mbunge wa Ruaraka Tom Kajwang’ ameitaka idara ya mahakama kupigana na ufisadi kwenye kitengo hicho, nje na ndani, ili kuimarisha imani ya umma.
Alisema kuwa sharti kila idara iwajibike, hasa idara muhimu kama ya mahakama, ambayo inahitaji kusimama kidede na kupigana na ufisadi.
Mbunge huyo alikuwa akiongea katika hafla moja ya wawakilishi wa bunge la Afrika ambalo ilijumuisha mawakili na wanasheria kwenye mkahawa mmoja jijini Mombasa, na aliongezea kuwa idara ya mahakama imeathirika na kuharibiwa heshima yake na baadhi ya wachache ambao wanajitakia makubwa
Mbunge huyo akiligusia suala la siasa za mmoja wa viongozi tanzu wa muungano wa upinzani alisema kuwa masaibu yanayomkumba seneta Moses Wetangula ni mbinu kutoka kwa wapinzani wake kutaka kumumaliza kisiasa, na kuwambia kuwa wamechelewa.
Aliwaambia wazi wale wana nia ya kumwangusha seneta Wetangula kuwa hawatafaulu kamwe, na chama cha upinzani kitasimama kidede kumtetea seneta huyo.
Alisema kuwa siasa za kubomoa ndizo zimekuwa zikichezwa humu nchini, na kusema wapo tayari na kamwe hawatatishwa na mbinu za upande wa serikali kutaka kumaliza nguvu za chama hicho cha upinzani.
Mkutano huo ulianza siku ya Alhamisi na unalenga kuendelea kwa siku mbili kwenye hoteli ya White Sands Hotel jijini Mombasa na umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika.