Kinara mwenza wa Cord ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Wiper, Bwana Kalonzo Musyoka, anatarajiwa kuzuru Mombasa siku ya Ijumaa.
Bwana Musyoka atazuru eneo hilo ili kuandaa kikao na jamii ya Wakamba katika kaunti hiyo.
Kulingana na waandalizi wa shughuli hiyo, Kalonzo atakaribishwa mjini Mombasa na Gavana Hassan Joho ambaye anatarajiwa kurudi nchini hii leo (Ijumaa), pamoja na Seneta wa Mombasa Hassan Omar na Mbunge wa Nyali Hezron Awiti.
Katika mahojiano na gazeti la The Star siku ya Alhamisi, Bwana Solomon Kuti, ambaye ni mwenyekiti wa kongamano la jamii za Mombasa, alisema viongozi hao watatu watawahutubia jamii ya Wakamba linaloishi eneo la Mombasa.
Bwana Kuti alisema kuwa viongozi hao watazungumzia kuhusu jinsi ya kuinua uchumi wa eneo la Ukambani na Mombasa kwa jumla.
"Hatutarajii siasa kupewa kipau mbele katika mkutano huo. Ajenda kubwa itakuwa kuiwezesha jamii na kushinikiza uwepo wa amani na umoja,” alisema Kuti.
Hassan na Awiti wanatarajiwa kuchukua fursa hiyo kutafuta uungwaji mkono wa kuwania kiti cha ugavana kwa tiketi ya Wiper.