Kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Mombasa Peterson Mailu amewaonya vijana dhidi ya kuvamia watalii hasa msimu huu wa likizo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mailu amesema kuwa vijana wanaopanga kuwavamia na kuwaibia wananchi pamoja na watalii ambao wanazidi kumiminika katika mji huo kwa ajili ya likizo ya mwisho wa mwaka watakabiliwa vilivyo.

“Tutawaandama mpaka tuwamalize wanaotuharibia utalii wa sehemu hii,” alisema Mailu.

Haya yanajiri baada ya kijana mmoja kuuawa kwa kupigwa risasi katika mtaa wa Bondeni, baada ya kujaribu kumuibia afisa wa polisi aliyekuwa amevaa nguo za raia.

Mailu alisema kwamba wataanza kuweka maafisa wasiovalia sare za polisi kwenye maeneo tofauti, ili kuhakikisha kuwa usalama wa hali ya juu unadumishwa.

Juma lililopita, Kamishna wa Mombasa Evans Achoki alisema kuwa maafisa wa usalama watashirikiana kuhakikisha kuwa kaunti nzima inabaki kuwa salama wakati huu wa likizo ndefu.

“Lazima tuangamize uahalifu katika kaunti nzima ya Mombasa,” alisema Achoki.