Huku uteuzi wa Makurutu ukikamilika Jumatatu, Kamanda ambaye alisimamia zoezi hilo katika eneo la Kitutu Chache kwenye Uga wa michezo wa Gusii alizua kicheko cha kufunga siku alipofunua kuwa makurutu hutumia Pikipiki kukimbia wakiachiliwa peke yao kukimbia barabarani.
Kamanda Fredrick Kagai alikuwa anajibu swali ambalo aliulizwa na mmoja wa Waandishi wa Habari kuwa ni kwa nini akaamua Makurutu wakimbie ndani ya uwanja kinyume na ilivyokuwa miaka zilizopita ambapo Makurutu walitumia barabara za mjini Kisii na kumalizia uwanja wa Gusii ndiposa akajibu kwa kusema kuwa Makurutu huenda pale nje na kupanda Pikipiki kuwazungusha alafu wanaletwa kwenye hilo lango kuu la uga wa Gusii na kujidai washindi.
"Tuliamua Wakurutu wakimbie humu ndani na pia tufanyie uteuzi huu humu ndani ya uwanja kwa sababu Makurutu wanapokimbia pale nje barabarani baadhi yao tuligundua wanatumia Pikipiki ili wamalize haraka, kitendo ambacho sio haki kwa wengine,” alidai Kamanda Kagai huku akiwasababisha Waandishi wa habari pamoja na Maafisa wengine waliokuwa naye kuangua kicheko.
Hata hivyo aliwashukuru Makurutu wote waliohudhuria uteuzi huo na kuwasihi waliokosa nafasi katika mwaka huu kujaribu tena mwaka ujao. Hata hivyo kulishuhudiwa idadi ndogo sana ya waliojitokeza kwenye zoezi hilo kulinganishwa na lile la miaka zilizopita.
Makurutu 26 walipenya katika kituo hicho cha Uga wa michezo wa Gusii ambapo vijana wa kiume waligawana 2/3 dhidi ya thuluthi moja ya kike kulingana na katiba ya Kenya.