Mwakilishi wa wadi ya Kamara katika bunge la kaunti ya Nakuru Joseph Ngware ametishia kuongoza wananchi kuweka matuta katika maeneo ambayo ajali zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret iwapo idara husika haitachukua hatua za haraka.
Wakiongea siku ya ijumaa katika eneo la Mau Summit baada ya mtoto wa miaka 11 aliyekuwa akivuka barabara kugongwa na gari na kufariki papo hapo, wakaazi wanaoishi katika baadhi ya vituo vya kibiashara kwenye barabara hiyo wamelalamikia ongezeko la ajali huku wakiitaka mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa barabara kuu kuweka matuta yatakayodhibiti mwendo wa magari na kupunguza visa ajali.
Wenyeji wa maeneo ya Mau Summit, Jogoo, Total na Kibunja wamesema zaidi ya watu sita wamegongwa na magari yanayoendeshwa kwa mwendo wa kasi katika muda wa majuma matatu.
“Sasa hapa pamegeuka na kuwa Limuru, hatukosi kuzika mtu kila mwezi. Mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa barabara kuu iliaahidi kuweka matuta hapa lakini haijatimiza, na kila wakati tukiripoti hakuna hatua inayochukuliwa,” akasema Jonathan Mwangi, ambaye ni mkaazi mmoja.
Mkaazi mwingine aliyejitambulisha kama James, alisema; “Hapa kuna kanisa, kuna shule ya msingi, na mbili za upili, na licha ya kujua hayo, hawakuweka matuta wakitengeneza hii barabara kuu”.
Mwakilishi wadi Ngware alisema haistahili kwa serikali kushuhudia maafa mengi ndiposa eneo hilo liwekwe matuta.
“Tumekuwa tukiandamana na sasa tumechoka. Tutajiwekea hayo matuta wenyewe wakikataa. Maisha ya binadamu ni muhimu kuliko malori yanayopita kupeleka bidhaa Uganda.”