Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amesema wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa hawataruhusiwa kuhudumu katika soko jipya la Kongowea.

Awiti amesema lazima utaratibu mwafaka ufuatwe ili kurahisisha shughuli sokoni humo, huku akitoa onyo kwa wenye nia ya kutumia njia za mkato kufanya biashara.

Akizungumza alipozuru soko hilo siku ya Jumatano, Awiti alisema wataanda mkutano pamoja na viongozi wa kiusalama mjini Mombasa ili kuunda kamati maalum ya kusimamia soko hilo.

“Hakuna mtu yeyote kutoka nje atakayekuja hapa na kudai kwamba yuko na biashara. Naibu kamishna katika kaunti ataongoza zoezi hilo akishirikiana na kamati itakayoundwa,” alisema Awiti.

Hata hivyo, aliongeza kwamba yeyote atakayefuata utaratibu uliowekwa ataruhusiwa kufanya biashara sokoni humo bila kujali kabila, dini wala sehemu anayotoka.

Aliongeza kwamba kamati hiyo ndio itakayotwikwa jukumu la kuhakikisha hakuna ubaguzi.

“Mfanyabiashara ni mfanyabiashara bora watu wetu ndio wanaofaidi. Nimezungumza na wenyekiti kuhakikisha kwamba kila mtu amepata nafasi yake,” aliongeza Awiti.

Mhandisi mkuu anayesimamia ujenzi huo Francis Murage, alisema soko hilo limejengwa kisasa ili kurahisisha shughuli za biashara.

“Hapa kuna vyoo vya kisasa, sehemu maalum ya kuegesha magari, nafasi kubwa za kufanyia kazi na pia sehemu maalum ya kuhifadhi uchafu wote unaotoka sokoni,” alisema Murage.

Soko hilo ambalo ndilo kubwa zaidi ukanda wa Pwani linatarajiwa kuwahudumia zaidi ya wafanyabiashara 1, 500.

Mradi huo umefadhiliwa na serikali kuu kwa ushirikiano na ile ya kaunti, na Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua rasmi jengo hilo pindi litakapokamilika.