Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu leba imetoa onyo kali kwa wawekezaji binafsi wanaofanya biashara humu nchini dhidi ya kuwanyanyasa wafanyikazi wao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea baada ya kuzuru kampuni ya kutengeneza nguo ya EPZ Hantex siku ya Ijumaa, kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo Jones Mlolwa ambaye pia ni mbunge wa Voi alisema kuwa ni lazima maswala ya wafanyikazi yazingatiwe kulingana na sheria.

Kamati hiyo imefanya ziara katika kampuni hiyo baada ya Mbunge wa Jomvu Twalib Badi kuwasilisha mswada bungeni ya kutaka kampuni hiyo kuwarejesha kazini zaidi ya wafanyikazi 400 waliofurushwa kazini kinyume cha sheria.

Katika hotuba yake kwa wafanyikazi hao waliokuwa wamefika kutoa malalamishi yao kwa tume hiyo, Badi alisisitiza kuwa kampuni hizo lazima zifaidi wananchi wa kawaida sawa na wanazozimiliki.

Inadaiwa kuwa kampuni hizo zimekuwa zikiwanyima wafanyikazi wake fursa ya kujiunga na vyama vya wafanyikazi, jambo ambalo wanakamati hiyo wamesema ni kinyume cha katiba.