Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo katika Wadi ya Esinse ilioko eneo Bunge la Mugirango Kaskazini katika Kaunti ya Nyamira Kennedy Ndege amekanusha madai ya wakaazi wa eneo hilo kusema pesa za Wadi hiyo hutumika vibaya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na Waandishi wa Habari mnamo siku ya Jumatano katika kijiji cha Rusinga, Ndege alikana madai hayo na kusema pesa za Wadi hiyo zinatumika vizuri, kufuatia ratiba ya Wadi hiyo.

Hii ni baada ya wakaazi hao kumkosoa Mwakilishi wa Wadi hiyo Teresa Nyaanga kwa kusema anatumia pesa za Wadi hiyo vibaya na kutofanya maendeleo katika eneo hilo.

“Katika Wadi ya Esinse tayari tumeweka taa tatu ambazo ziligharamia Sh750,000. Hii karatasi inapitishwa hapa na kusema tulitumia Sh25 millioni ni uwongo. Sh25 millioni zinatumika kuweka mataa katika Kaunti nzima ya Nyamira wala sio katika Wadi hii pekee,” alisema Mwenyekiti Ndege.

Kwa upande mwingine wakaazi wa Wadi hiyo wakiongozwa na Joseph Nyarang’o, utumizi mbaya wa pesa za Wadi hiyo umekuwa ukishuhudiwa sana kwa muda mrefu.

“Mradi wa maji katika sehemu ya Manga walisema walitumia Sh9 million, Taasisi ya Saiga Ngiya iligharamia Sh2.6 millioni kwa ujenzi, kununua pikipiki tatu ambazo zitasaidia madaktari wa kutibu mifugo wanasema zilichukuwa Sh8 millioni, kununua madawa ya kutibu mifugo pia iligharamia Sh8 millioni. Huo ni uwongo pesa maanake tunahisi kwamba pesa zinafichwa,” alidai Nyarang’o mkaazi wa Wadi ya Esinse.

Mwenyekiti huyo aliwaomba wakaazi hao kuwa watulivu, wenye subira na watafanyiwa maendeleo zaidi. Pia aliwasihi kuacha kuingiza siasa katika mambo ya maendeleo.