Kamati ya seneti kuhusu afya sasa inasema kuwa mizozo iliyopo katika sekta hiyo katika kaunti zote nchini inatokana na migogoro ya kila mara baina ya usimamizi na wahudumu wa afya.
Haya yameibuka wakati wa kufunguliwa kwa warsha ya siku mbili ya kamati hiyo katika hoteli ya Enashipai mjini Naivasha Jumatatu, ambapo washikadau katika sekta ya afya wanatarajiwa kutoa mapendekezo yao kwenye mswada wa afya.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohamed Kuti alisema kuwa; “Mswada huu utaangazia pakubwa utendakazi wa wahudumu wa afya pamoja na kushughulikia raslimali zao.”
Naye naibu wa mwenyekiti Bi Zipporah Kittony kwa upande wake alisema kuwa; “Tuko tayari kuwahusisha washikadau wote ili kuafikia sheria itakayowafaidi wote.”
Hata hivyo, muungano wa madakitari nchini -KMA- pamoja na chama cha wauguzi wameteta na kusema kuwa mapendekezo waliyoyatoa hayajawekwa kwenye miswada inayotayarishwa.
Wakuu hao Dkt Elizabeth Wala na Dkt Oluga Ouma walisema kuwa ni sharti maswala ya wahudumu wa sekta hiyo yaangaliwe ili sheria hiyo iweze kukubaliwa na wote.