Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amewataka viongozi mbalimbali wanaojumuisha kamati iliyobuniwa kuangazia swala la usalama kutekeleza majukumu yao bila ya kuogopa wala kuegemea upande wowote.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Maalim amesema kuwa kuna haja ya kamati hiyo kutembelea maeneo yanayoathirika zaidi na utovu wa usalama, ili kutathmini na hata kupata habari zinazowahusu wahalifu hao.

Akizungumza kwenye kikao na wawakilishi wa maeneo mbalimbali mjini Mombasa katika makao makuu ya polisi, Maalim alisisitiza kuwa wahalifu wote watakaopatikana na makosa na kamati hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kamishna huyo aliyataja maeneo ya Kisauni haswa Soko Mjinga, Mishomoroni na Katisha, kama yanayokumbwa na uhalifu zaidi.

“Wazee wa mitaa waliojumuishwa kwenye kamati hiyo watahitajika kuwasilisha ripoti kila wiki, ya namna kesi za uhalifu zilivyoripotiwa na kutatuliwa,” alisema Maalim.

Aidha, aliwapongeza viongozi wa siasa waliofika kwenye mkutano huo kwa kuapa kushirikiana na idara ya usalama ili kukomesha visa hivyo vinavyowafanya wengi wa wakazi wa Mombasa kuishi kwa hofu.

Akizungumzia kuhusu makundi ya vijana yanaosimamisha magari katika maeneo mbalimbali ya Bursheba huko Kisauni na kupora vipuri pamoja na vioo vya magari, Maalim alisema maafisa wa usalama wasio na sare watakuwa wakishika doria mchana na usiku ili kuregesha imani kwa wakazi wa maeneo hayo.

Maalim pia aliwashutumu wanaotetea makundi ya vijana wahalifu, kwa kusema kuwa atakayepatikana atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.