Huenda viongozi wa usalama katika Kaunti ya Mombasa wakalazimika kuvunjilia mbali kamati za usalama, al maarufu kama Nyumba Kumi, iwapo visa vya utovu wa usalama vitaendelea kukithiri katika kaunti hiyo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mohamed Maallim alisema kuwa kamati zinazohudumu kwa sasa zimelegeza kamba katika utendakazi wake, kutokana na ongezeko ya makundi ya uhalifu.
“Kamati mpya zitaundwa na kupewa mafunzo iwapo tutalazimika kuvunja kamati za sasa,” alisema Maalim.
Kamishna huyo aliwatahadharisha wanakamati hao dhidi ya kuzembea kazini, huku akiongeza kuwa serikali imeanzisha msako mkali dhidi ya watakaopatikana wakishirikiana na wahalifu.
Haya yanajiri baada ya kina mama kulalamikia kunyanyaswa kimapenzi na vijana wanaojihusisha na makundi ya uhalifu.