Kamati za shule mbalimbali katika kaunti ya Kisii zimeombwa kuripoti visa vya upikaji wa pombe haramu karibu na shule zao.
Hii ni baada ya kubainika kuwa kuna wagema ambao hupika pombe haramu karibu na shule huku wanafunzi wakibugia pombe hiyo kisha kuacha masomo.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Masimba, Nyaribari Masaba naibu kamishena wilayani Masaba Kusini Nzaria Gitonga aliomba kamati hizo za shule kuhakikisha visa hivyo vimeripotiwa ili hatua kali zichukuliwe dhidi ya wagema hao.
“Pombe haramu imekataliwa katika taifa letu la Kenya na iwapo kuna wagema ambao hupika pombe karibu na shule visa hivyo vimeripotiwa ili hatua mwafaka zichukuliwe,” alisema Gitonga.
Wakati huo huo, Gitonga aliomba wakaazi wote kushirikiana na machifu wa kaunti ya Kisii kupunguza upishi wa pombe haramu ambayo ni kinyume cha sheria.
“Naomba kila mkaazi kujaribu kila awezalo kuhakikisha hakuna pombe haramu vijijini kwa kushirikiana na machifu," aliongeza Gitonga.