Utoaji wa leseni za vilabu na unywaji wa pombe Nakuru unatarajiwa kuchukua mwelekeo mpya baada ya Gavana Kinuthia Mbugua kuzindua rasmi kamati za kudhibiti utoaji leseni za vileo kwenye kaunti ndogo zote, na kamati tawala ya kukagua usawa wa uamuzi wa kamati hizo.
Gavana Mbugua amesema kwamba sheria ya mwaka wa 2014 inayohusu udhibiti wa unywaji wa vileo katika kaunti ya Nakuru, inaruhusu utoaji leseni na udhibiti wa uzalishaji wa vileo, uuzaji, usambazaji na utangazaji wake.
Alisema serikali yake imeunda kamati hizo za kaunti ndogo na kuzipa majukumu ya utoaji leseni, pamoja na kukagua maswala yanayohusiana na ubora wa huduma anazotoa mwenye biashara hiyo kwa wateja wake mara kwa mara, ili kuhakikisha huduma hizo zinaendana na matakwa yaliyowekwa.
Ili kuweka uwazi wa swala hiyo, taarifa ya Kinuthia imesema kwamba idara ya biashara tayari imechapisha maelekezo yatakayoongoza kamati hizo wakati wa kutekeleza sheria hiyo.
Aidha, imebainika sasa kwamba leseni zitakazotolewa zitakuwa za viwango tofauti, kulingana na biashara ya mtu binafsi, kuanzia wanaouza pombe kiwango kidogo, wasambazaji, wanaouza pombe kwa wanabiashara wa chini, wanaotengeza vileo na wanaouza klabu, kati ya zingine.
“Nahakikishia wawakilishi wa serikali kuu, sekta ya kibinafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na washikadau wengine kujikakamua ili serikali yangu kushirikiana nanyi na kufanya kazi kama kikosi kimoja," alisema Mbugua.
Alisema kuwa hilo litasaidia kupigana na pombe haramu na dawa za kulevya katika kaunti ya Nakuru.