Shirika la huduma za feri KFS, limesema kuwa litaweka kamera za CCTV katika kila feri inayohudumia umma, ili kuwanasa wanaume wanaodaiwa kuwadhulumu wanawake kimapenzi katika kivuko cha Likoni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake siku ya Jumanne, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Bakari Ngao, alidokeza kuwa hatua hiyo inanuia kutokomeza lalama za kila mara kutoka kwa wanawake wanaodai kudhulumiwa kimapenzi.

“Kamera hizo zitatusaidia kuwatambua wale ambao wanaendeleza tabia hiyo mbaya ya kuwadhulumu wanawake kimapenzi. Yeyote atakayepatikana na hatia atashtakiwa,” alisema Ngao.

Hata hivyo, afisa huyo alisema kuwa itakuwa vigumu kutenga maeneo maalum kwa wake na waume kwenye feri za Mombasa, au hata kuweka feri mahususi za kubeba watu wa jinsia moja pekee.

“Hatua hiyo itapoteza muda na kusababisha msongamano katika feri, na hata kulemaza huduma za shirika hili,” alisema Ngao.

Haya yanajiri baada ya bunge la kaunti ya Mombasa kupitisha hoja linalopendekeza wanaume na wanawake kutengewa sehemu tofauti katika feri, kufuatia malalamishi ya kila mara kutoka kwa wanawake kuwa wanadhulumiwa kimapenzi na wanaume ndani za feri hizo.