Kamishina wa kaunti ya Nyamira Josephine Onunga amehimizwa kuongoza maafisa wa polisi hadi wilaya ya Nyamira Kaskazini ili kumwaga pombe haramu ambayo imekita mizizi katika eneo hilo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa machifu na maafisa wa polisi wanakusanya pesa kutoka kwa wagema na kutomwaga pombe hiyo haramu huku Onunga akiombwa kuongoza shughuli hiyo.
Wakizungumza mjini Nyamira mwenyekiti wa chama cha akina mama kwa jina Foundation for Human Rights Kenya Lillian Nyamweya alisema kuwa upikaji wa pombe umeongezeka wilayani Nyamira Kaskazini na kuomba kamishina kuongoza umwagiaji wa pombe hiyo kwani umeathiri vijana wengi.
“Hapa Nyamira shughuli ya upikaji wa pombe haramu inaendelea kila wakati na machifu na polisi hawajafanya chochote ata tumeshindwa cha kufanya,” alisema Nyamweya.
“Vijana wetu wanabugia pombe haramu na rais mwenyewe alikashifu swala hilo lakini hapa Nyamira utovu huo unaendelea, tunaomba kamishina atusaidie ili pombe haramu imwagwe,” aliongeza Nyamweya.