Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imeshikilia msimamo wake wa kuangamiza makundi ya uhalifu hasa eneo la Kisauni.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed, amesisitiza kuwa watahakikisha wahalifu wote wamemalizwa katika eneo bunge hilo.
Akizungumza siku ya Ijumaa kwenye baraza la kujadili usalama eneo la Kadongo, Kisauni, Maalim aliwahimiza wakaazi kushirikiana na idara ya usalama katika kuwafichua wahalifu ili kuwawezesha polisi kuwachukuliwa hatua za kisheria.
“Siku za uhalifu ziko karibu kuzikwa kwenye kaburi la sahau kwani tutakabiliana na magenge ya uhalifu vilivyo,” alisema Maalim.
Eneo la Kisauni limekuwa likigonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kufuatia kukithiri kwa visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na vijana wenye umri mdogo, waliojihami kwa silahi.
Kundi la Wakali Kwanza, ambalo limekuwa likiwahangaisha wakaazi wa Kisauni pia linadaiwa kuwadhulumu wanawake kimapenzi kwa kuwanyonya matiti.