Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Mohamed Maalim ameahidi kuimarisha vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati katika kaunti hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Maalim ameahidi kupambana na mabwenyenye wanaoshiriki biashara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliowaleta pamoja viongozi mbalimbali kutoka idara ya usalama katika afisi yake mjini Mombasa, Maalim alisema kuwa ulanguzi wa mihadarati Pwani ndio changamoto kuu inayochangia ongezeko la vijana kujishuhulisha visa vya uhalifu.

Maalim aidha amewataka washikadau katika idara ya usalama mjini Mombasa kuwa macho zaidi.

“Wanaotekeleza biashara ya mihadarati ni mabwenyenye ambao huwatumia vijana walioacha shule kutokana na changamoto za kifedha wanazokumbana nazo, kisha wanapokamatwa huwatetea ili wazidi kuendesha biashara hiyo,” alisema Maalim.

Kwa upande wa usalama mashinani, Maalim amewataka machifu kuwahimiza wazazi kushirikiana na idara ya usalama ili kuwanasua wanawao kutoka kwenye janga la mihadarati.