Polisi katika Kaunti ya Mombasa wameahidi kutoa usalama wa kutosha kwa mabalozi wa mpango wa Nyumba Kumi.
Hii ni baada ya idara ya usalama kupokea visa kadhaa vya mabalozi hao kuvamiwa na wahalifu na hata wengine kuuawa.
Akizungumza katika mkutano na wananchi mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kamishna wa Kaunti Maalim Mohamed alisema wamepokea visa viwili vya mabalozi hao kuuawa.
“Niliambiwa hapa sehemu ya Faya kuna mabalozi wawili waliwahi kujitolea lakini mwishowe wakauawa. Mambo haya hayatajirudia tena,” alisema Maalim.
Maalim alisema mradi huo ulizinduliwa na serikali ya kitaifa kama njia moja ya kuimarisha usalama kote nchini, na kuongeza kuwa visa vya mabalozi kuvamiwa haviwezi kuzuia oparesheni hiyo kuendelea.
Hata hivyo, aliwashauri mabalozi hao kutoingiwa na hofu kwani idara hiyo sasa imeweka mikakati ya kutosha kuwapa ulinzi.
Wakati huo huo, afisa huyo alitoa nambari zake za simu kwa wananchi na kuwasihi kumpigia simu moja kwa moja iwapo watashuhudia jambo lolote linalotishia usalama.
Maalim alitoa kauli hiyo baada ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kutaka kuelezwa ni jinsi gani serikali itawalinda viongozi hao wa mashinani, huku wakilalamika kwamba utovu wa usalama umewafanya kuogopa kujitokeza.
Hata hivyo, kamishna huyo alijipata katika hali ngumu pale wananchi walipomuuliza iwapo serikali ina mpango wowote wa kuanza kuwalipa mabalozi hao mishahara, kama wafanyikazi wengine wa umma.
“Serikali ina mpango huo lakini pia mjue kwamba iwapo hatua hiyo itatekelezwa itabidi wananchi pia tulipe ushuru zaidi ya vile tunalipa saa hii,” alisema Maalim.
Mkutano huo wa kiusalama ulifanyika katika uwanja wa Fort Jesus mjini Mombasa, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria ikiwemo kamati maalum ya usalama Mombasa, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir miongoni mwa wengine.