Watengenezaji na wauzaji wa pombe haramu katika Kaunti ya Uasin Gishu wameonywa kwamba wataadhibiwa iwapo hawataicha biashara hiyo haramu.
Akuzunguza katika uwanja wa 64 mjini Eldoret wakati wa maadhimisho ya sherehe ya Jamuhuri siku ya Jumamosi, kamishma wa kaunti hiyo Abdi Hassan alisema kuwa yeyote atakayepatikana akiendeleza biashara hiyo atadhibiwa vikali kwa mujibu wa sheria.
"Pombe haramu inaadhiri vijana wengi, imesababisha vifo hapa nchini na kwa hivyo tutakabiliana vikali na wanaoendesha biashara hii katika kaunti ya Uasin Gishu," alisema Hassan.
Aidha aliwaomba wananchi kushirikiana kutoa taarifa kwa maafisa wa usalama kuhusiana na biashara hii.
Vilevile kamishna huyo ametoa wito kwa wazazi kuwa waangalifu na kuchunguza mienendo ya wanao haswa wakati huu wa msimu wa sherehe ili kuwaepusha kujihusisha na unywaji wa pombe na utumiaji mihadharati.
"Msimu huu, wazazi wanapaswa kuwa waangalifu na kutazama mienendo ya wanao, tusije tukawa na kesi kama za hapo awali ambapo watoto walipatikana katika sehemu ya burudani hapa mjini Eldoret wakijihusisha na mambo yasiostahili," alisema Hassan.