Mpango wa serikali kusajili wapiga kura hadi mashinani maarufu 'Mobile ID Registration' umepongezwa pakubwa.
Naibu kamishna wa manispaa Nakuru Catherine Njoroge katika mahojiano ya kipeekee na mwanahabari huyu Jumatano alisema kuwa mpango huo wa kuzuru mashinani na kusajili wananchi kupata vitambulisho vya kitaifa ni hatua mwafaka.
Kwa mujibu wake, mpango huo umerahisisha shughuli hiyo na pia kupunguza msongamano katika vituo vya Huduma centre.
"Tumekuwa tukishuhudia msongamano si haba kule Huduma Centre, hivyo basi hatua hii ya usajili mashinani ni muhimu sana," alisema Njoroge.
Wakati huo huo, alisisitiza ujumbe kwa umma kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kujisajili kwa wingi kupata vitambulisho vya kitaifa.
Kwa mujibu wa Naibu kamishna huyo, kila mwananchi aliyetimu miaka 18 anafaa kuwa na kitambulisho cha kitaifa.
"Wito wangu kwa wakazi wa manispaa hii ni kwamba wakumbatie mpango huu na kila kijana aliyetimu miaka 18 ajisajili kupata kitambulisho cha kitaifa," alisisitiza afisa huyo.
Wakati huo huo alisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na maafisa wa utawala katika vita dhidi ya pombe haramu.