Wapishi 10, wa pombe haramu kutoka eneo la Legetio na Lengenet wamezuiliwa katika kituo cha Polisi cha Rongai wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Wapishi hao walikamatwa kwenye oparesheni iliokuwa imeongozwa na D.O wa Rongai, machifu, maafisa wa polisi na wazee wa Nyumba Kumi Alhamisi jioni.
Kwenye oparesheni hiyo Lita 600 na Lita 120 za chang'aa za 'kangara' zilinaswa.
DC wa Rongai David Koskei amesema kuwa, wapishi hao wa pombe haramu wanashukiwa kuwa ndio waliowavamia wazee wa Nyumba kumi kwa mishale na mapanga siku ya Jumapili wiki iliyopita.
“Hawa wapishi wa pombe hizi haramu ndio waliowashambulia wazee siku ya Jumapili na tutahakikisha wanachukuliwa hatua kali kisheria na lazima tutamaliza upishi wa pombe na unywa katika Rongai, ikiwa sisi wote tutashirikiana,” alisema Bw Kosgei akiwahutubia wanahabari.
Aliwapongeza wananchi akisema kwamba walisadia pakubwa afisi yake na habari muhimu ambazo zilifanikisha oparesheni hiyo kufaulu.
Aidha alitangaza rasmi vita dhidi ya pombe haramu kwenye kaunti ndogo ya Rongai.