Kufuatia watoto watano wa darasa la chekechea kufariki kwenye ajali ya barabarani kwenye mzunguko wa barabara ya Awasi kwenye barabara kuu ya Kisumu-Kericho siku ya Jumanne, sasa kamishna wa kaunti ya Nyamira amejitokeza kuwahimiza madereva kuwa waangalifu barabarani. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu kamishna, Onunga alisema kuwa yafaa madereva kuwa waangalifu wanapoendesha magari ili kulinda maisha ya wananchi barabarani. 

"Hatutaki kuona maafa tunayoendelea kuyashuhudia kwenye barabara zetu na ndio maana nawahimiza madereva kuwa waangalifu barabarani ili kulinda maisha ya wasafiri na hata wapita njia," alisema Onunga.

Onunga aidha aliongeza kusema kuwa hatosita kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva watakaopatikana kukiuka maagizo ya barabarani. 

"Madereva wasiozingatia sheria za barabarani kamwe hawatovumiliwa, na nitahakikisha kwamba wamekabiliwa kisheria kwa maana hatuwezi keti tuwe tukiangalia watu wetu wakiangamia kwa sababu ya uendeshaji magari na watu wasiozingatia sheria za barabarani," aliongezea Onunga.