Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewaonya vikali machifu na manaibu wao wanaoruhusu ugemaji wa pombe haramu katika maeneo yao ya utawala.
Kwenye kikao na wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatano, Onunga alisema kuwa afisa yeyote wa utawala atakaye patikana akiruhusu ugemaji huo kuendelea atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
"Ugemaji na ubugiaji wa pombe haramu ni hatia katika sheria za taifa hili, na ndio maana nawaonya vikali machifu na manaibu wao watakaopatikana wakiruhusu ugemaji huo kuendelea kuwa watachukuliwa hatua kali za kinidhamu," alisema Onunga.
Onunga aidha aliongeza kwa kuwaonya vikali watu wanaoajiri watoto ili kufanya kazi za sulubu huku akisema kuwa watoto wana haki ya kupata masomo.
"Nimepokea ripoti kwamba kuna watu wanaoajiri watoto ili kuwafanyia kazi za nyumbani. Nataka watambue kuwa ajira kwa watoto ni kinyume cha sheria na yeyote atakayepatikana atakabiliwa kisheria,” aliongezea Onunga.