Kamishna wa kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amejitokeza kuwaonya vikali wamiliki wa vyumba vya vileo almaarufu baa dhidi ya kuwaruhusu watoto wa chini ya miaka 18 kunywa pombe kwenye maeneo yao ya burudani.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumapili, Onunga alisema kuwa ni hatia kisheria kwa wamiliki wa baa kuwaruhusu watoto kunywa pombe kwenye maeneo yao ya biashara, huku akionya kuwachukulua hatua za kisheria.
"Ni hatia kwa wamiliki wa baa kuwaruhusu watoto wa chini ya umri wa miaka 18 kunywa pombe kwenye baa zao, na yeyote atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria," alionya Onunga.
Onunga aidha aliwahimiza wazazi kuchukua hatua ya kushauri wanao kujiepusha na tabia zinazoweza kuathiri maisha yao.
"Kwa sasa shule nyingi zimefungwa na watoto wengi wapo nyumbani, na ni himizo langu kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanatenga muda kuwashauri wanao kujiepusha na tabia zinazoweza kuathiri maisha yao," aliongezea Onung'a.