Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewaonya vikali wanasiasa wanaoenda kwenye ofisi za usajili wa vitambulisho ili kuchukua vitambulisho vya kitaifa kwa niaba ya wakazi wa maeneo yao.
Akiwahutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatano, Onunga alisema kuwa kwa muda amekuwa akipokea malalamishi kutoka kwa maafisa wa usajili wanaoangaishwa na wanasiasa wenye nia ya kuchukua vitambulisho kwa niaba ya wapiga kura wao.
"Kitambulisho ni stakabadhi muhimu sana kote ulimwenguni na sheria iliyoko ni kuwa anayejisajili kupokea kitambulisho hicho ndiye anayestahili kuenda kukichukua baada ya muda fulani. Iwe onyo kwa wanasiasa wanaohangaisha maafisa wa usajili kwa kutaka kuchukua vitambulisho kwa niaba ya wapiga kura wao," alisema Onung'a.
Onung'a aidha aliwarai wananchi kutokubali kuuza vitambulisho vyao kwa wanasiasa huku akisema kuwa kitambulisho ndio stakabadhi muhimu inayomwezesha mwananchi kujisajili maka mpiga kura.
"Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao na huenda kuna wanasiasa wenye nia ya kununua vitambulisho kutoka kwa wananchi ili wasiruhusiwe kupiga kura. Ni ombi langu kwa wananchi kutokubali kuuza vitambulisho vyao kwa kuwa hiyo ndiyo silaha itakayowawezesha kuwaondoa ofisini mwanasiasa wazembe," aliongezea Onung'a.