Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amewakashifu wale wanaoendeleza fitina kuhusu kuwepo kwa uhasama wa kimaendeleo baina ya serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza Jumamosi alipozuru mradi wa ujenzi unaoendeshwa na serikali katika soko la Kongowea, Bw Mohamed alisema mradi huo utaimarisha huduma za soko kwa wakenya wote huku akilitaja soko hilo kama soko bora zaidi nchini ambalo ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi milioni 300.

Mohamed alieleza kuwa hakukuwa na mvutano wowote baina ya serikali hizo mbili kutokana na mradi huo, hili likiwa ni kufuatia taarifa za kuwepo kwa ushindani wa ni nani anayegharamia ujenzi huo baina ya serikali hizo mbili.

Kamishna huyo alidokeza kuwa mradi huo ulianzishwa na rais mstaafu Mwai Kibaki na kuwa unakamilishwa na rais Kenyatta kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ili kuwahakikishia wananchi huduma bora.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Julai hii kufuatia ahadi za rais Kenyatta mapema mwaka huu alipokuwa katika ziara yake ya Pwani.