Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed anatarajiwa kuandaa kikao na idara ya mazingira kutafuta suluhu ya jaa la Kibarani linalotajwa kuwa kero kwa watalii.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Maalim amesema amepokea malalamishi mara kadhaa kutoka kwa wadau mbalimbali, haswa kutokana na kukithiri kwa moshi kila siku katika sehemu ya Kibarani, wakati wa kuchomwa taka.

Maalim alisema kuwa tatizo la taka limeonekana kuwa changamoto katika mji huu wa kitalii, ambao ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaozuru kanda ya Pwani.

“Suala la taka katika jiji hili limekuwa changamoto kubwa na hatutokaa kama viongozi tukilitazama. Tumezungumza na katibu wa kaunti na tutafanya kikao kujadili suala hili,” alisema Maalim.

Wakati huo huo, mkurugenzi wa Hoteli za Heritage na mwenyekiti wa chama cha wadau wa utalii Pwani Mohamed Hersi, ameunga mkono kauli hiyo akisema moshi mwingi unaotoka katika sehemu ya Kibarani umekuwa kero kwa watalii wanaotumia barabara hiyo kutoka na kuelekea uwanja wa ndege wa Moi.

“Kibarani bado ni shida kwetu na kumekuwa na moshi ambao unawahaingaisha sana walipa ushuru,” alisema Hersi.

Haya yanajiri wakati ambapo kumekuwa na malalamishi kuhusu moshi unaotoka katika jaa la Kibarani, unaotajwa kuwa kero kwa wengi haswa wakaazi wa mitaa jirani.