Kamishna mpya wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed ametoa wito kwa wananchi pamoja na viongozi wa kaunti hiyo kushirikiana naye kikamilifu ili kuhakikisha usalama unaimarika katika eneo hilo.
Mohamed ambaye ana takriban majuma mawili tangu kuhamishwa Mombasa kutoka kaunti ya Bungoma, amesema ushirikiano pekee baina ya pande hizo ndio utatoa suluhu ya changamoto zinazoikabili kaunti ya Mombasa, ikiwemo suala la usalama na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana.
Akizungumza ofisini mwake siku ya Jumanne, Mohamed alisema ataendeleza mikakati thabiti kwa ushirikiano na viongozi ili kuona kuwa kuna ubora wa huduma kwa wakaazi.
“Nimewahi kuhuduma katika eneo hili kwa hiyo mimi sio mgeni. Nahitaji tu ushirikiano baina ya wananchi na viongozi,” alisema Mohamed.
Ikumbukwe kuwa kaunti ya Mombasa kwa mara kadhaa imewahi kugonga vichwa vya habari kutokana na kuchipuka kwa makundi yenye misimamo mikali pamoja na mauaji ya kiholela ya wahubiri wa kidini yanayodaiwa kutekelezwa na watu wasiojulikana.
Kamishna huyo aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Wilaya wa Mombasa katika kipindi cha mwaka 2004 hadi 2007, kabla kwenda masomoni na kisha baadae kuhamishwa hadi Kaunti ya Bungoma kama kamishna wa kaunti hiyo.